12 Agosti 2026 - 21:00
Waziri wa Mambo ya Ndani Pakistan: Uhusiano Imara wa Tehran na Islamabad Ugeuzwe Kuwa Matokeo ya Kivitendo

Mohsin Naqvi amesema uhusiano wa kina kati ya wananchi wa Iran na Pakistan unapaswa kuzaa ushirikiano zaidi na matokeo ya kivitendo, akisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi za pamoja katika kufikia malengo ya nchi hizo mbili.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi, amesema uhusiano na mafungamano ya kina yaliyopo kati ya wananchi wa Iran na Pakistan yanapaswa kutafsiriwa katika kuimarisha ushirikiano na kufikia matokeo ya kivitendo yanayowanufaisha wananchi wa nchi hizo mbili.
 
Naqvi ameyasema hayo katika mkutano wake na Mohsen Rezaei, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo pia alimpongeza Rezaei kwa kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo mpya.
 
Waziri huyo wa Pakistan pia aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Waziri Mkuu na Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, akisema anaamini uzoefu, busara na uwezo wa kiakili na kiuongozi wa Rezaei vinaweza kuchangia katika kuweka msingi wa usalama na amani endelevu katika eneo.
 
Naqvi ameeleza kuwa uhusiano kati ya Tehran na Islamabad unaendelea kukua kwa kasi, akisisitiza kwamba mahusiano ya Iran na Pakistan yamekuwa mazuri kwa muda mrefu, lakini katika miezi ya hivi karibuni yamefikia kiwango cha juu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
 
“Leo tunashuhudia kiwango cha uhusiano ambacho hakikuwepo hapo awali,” alisema Waziri huyo, akielezea kuimarika kwa uhusiano wa pande mbili.
 
Aidha, Naqvi ameeleza kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupongeza juhudi za Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mambo ya Ndani wa Iran, akitaja nafasi yao kuwa muhimu katika kuendeleza na kuimarisha uhusiano kati ya Tehran na Islamabad.
 
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan pia ameangazia mshikamano na hisia za karibu zilizopo kati ya wananchi wa Iran na Pakistan, akisema mshikamano huo umeonekana kwa kiwango kikubwa kupitia kuandaliwa kwa hafla kubwa nchini Pakistan ya kuadhimisha kuuawa shahidi kwa kiongozi wa Muqawama wa Mapinduzi ya Kiislamu.
 
Naqvi amesisitiza kwamba uhusiano huo wa kina na mafungamano kati ya wananchi wa Iran na Pakistan unapaswa kuzaa ushirikiano zaidi na matokeo yanayoonekana kwa vitendo.
 
Amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuongeza mawasiliano, utekelezaji na juhudi za pamoja ili kufikia malengo ya nchi hizo mbili.
 
Waziri huyo amesema anaamini kuwa Iran na Pakistan zina uwezo wa kufikia malengo yao ya pamoja, kutokana na dhamira na utashi wa kisiasa unaoonyeshwa na viongozi na maafisa wa nchi zote mbili.

Waziri wa Mambo ya Ndani Pakistan: Uhusiano Imara wa Tehran na Islamabad Ugeuzwe Kuwa Matokeo ya Kivitendo

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha